300x250 AD TOP

Template information

Thursday, 22 May 2014

Tagged under:

The Second Door- Episode 2


Mpenzi msomaji katika Episode iliyopita, tumeona jinsi ambavyo taarifa tata za hukumu ya kifo zilivyomfikia Frank na jinsi alivyo zipokea. Sio kwamba tu taarifa zile zilimstua bali zilimchanganya kwa kiasi kikubwa sana. Saa nne Asubuhi Frank anakata tiketi na kupaa kurudi Tanzania, Pengine unaweza kujiuliza kwanini Frank aliamua kuondoka Kazini bila kuomba ruhusa! Lakini ukweli ni kwamba Mlolongo wa kuomba ruhusa ungeweza kumgharimu zaidi ya siku 5, kwa mantiki hiyo basi Frank hakuona sababu ya kuingia kwenye mzunguko huo.

Huku Tanzania Mrembo Brenda anajaribu kumpigia simu frank kwa mara nyingine ili ajaribu kumueleza kinachoendelea, lakini safari hii simu ya Frank Haipatikani kabisa. Brenda anawaza na kuwazua. Baadae anapata wazo la kujaribu kwenda kuzungumza na mama ili wakusanye nguvu waende Ofisi ya Umoja wa mataifa kitengo cha haki za binadamu kujaribu kuelezea hali halisi na kuomba msaada. Wazo la kwenda kwa mama lisingekuwa rahisi sana kwa Brenda lakini msongo wa mawazo aliokua nao haumpi shida mrembo huyu kutekeleza wazo lolote linalomjia kichwani kwake.

Kufumba na kufumbua Brenda anaingia nyumbani kwa kina Tarick, Kitendo cha kuingia sitingroom anagongana macho uso kwa uso na mama, mama anaonekana kama mtu aliekuwa analia, lakini kitendo cha kumuona Brender Ghafla kinamfanya apigwe na butwaa na uso mzima unamkauka kwa tahamaki. Kwa hasira mama anasema, “Umefata nini ……. Umefata nini hapa nakuuliza! Baradhuri mkubwa wewe usiekuwa na haya, Yaani bado hujaridhika tu, mpaka unathubutu kukanyaga tena humu ndani?”.

Kauli hizo kali zinamfanya Brenda anaangua machozi mpaka kamasi jepesi linamtiririka, anajaribu kuongea,”Tafadhari mama nakuomba unisikilize, mimi sikupanga haya yote yatokee”, Kauli hiyo ya Brenda inaishia kumpandisha hasira mama kwa ukali anamkatisha na kusema,”Mshenzi mkubwa wewe, tena ishia hapo hapo……… nikusikilize uniambie nini! Mwanangu Tariki si alikusikiliza wewe! Nini umempa?”. Bado Brenda anazidi kumsihi na kumbembeleza mama kwa kusema,”Halikuwa lengo langu haya yote yatokee mama yangu, naomba unisamehe tafadhari” , Kauli nyepesi, kilio na huruma kubwa anavyoionesha Brenda bado havifui dafu dhidi ya hasira za mama, kwa ghadhabu anamjibu,”kama haikua dhamira yako unaomba samahani ya nini?”, baada ya kuhoji mama anakaa kimya kidogo huku Brenda akiendelea kulia, mama anaendelea kwa kusema, ”sasa…. Naomba utoke nyumbani kwangu, nenda kaombe msamaha Mahakamani ulipotoa ushahidi kuwa Tariki ni gaidi, ukasema Tariki ni muuaji……..” mama anaendelea kuongea maneno hayo kwa hasira huku akilia kwa sauti, ”wewe si ndio ulitoa ushahidi kuwa Tariki anashirikiana na wasomali weweee…..! umesababisha mwanangu ahukumiwe kifo sio wewe!? Namtaka mwanangu……. Namtaka Tariki wangu mimi........, Toka kamlete Tariki wangu, toka sasa hivi kaniletee mwanangu……. Nenda kaombe samahani mahakamani, kawaambie uliwadanganya ”.

Mama anaongea maneno hayo kwa hasira huku akilia kwa uchungu, Brenda nae huku akiwa anatimuliwa na mama anasema,”Unanihukumu kwa kosa lisilokuwa langu mama yangu…………….”. Mama na Brenda wanakosa maelewano, Brenda anafukuzwa na kuondoka.

Akiwa safarini kurudi Tanzania Frank alighubikwa na mawazo, alifikiria sana kuwa inawezekanaje Tariki huyu anaemfahamu kuwa hawezi hata kuua panya, leo hii akahusike kwenye tukio lakuua mamia ya watu. Akafikiri kuwa inawezekana kwamba ugumu wa maisha na tamaa ya mali ndivo vilivyo mchochea mpaka kudumbukia kwenye Vitendo hivyo Haramu!. Hayo na maswali mengine mengi sana alijiuiza Frank, akawaza na kuwazua bila kupata majibu stahiki mpaka kichwa kikaanza kumuuma.

Akiwa amerudi nyumbani kwake, baada ya kutafakari sana Brenda anajipa jibu kuwa ni kweli kwamba yeye ndie aliyesababisha hukumu ya Tarick, Brenda anafikiria sana na kufikia hatua ya kuamua kuwa, kwa kosa kubwa ambalo amelifanya, la kusababisha hukumu ya kifo cha mtu asiekuwa na hatia, hata yeye hastahiri kuendelea kuishi. Brenda anaingia chumbani kwake na kuchukua picha kubwa ya Tarick, Huku machozi yakimtoka……. Anasema moyoni mwake,”Tarick mpenzi wa moyo wangu……… nasikitika kwa yote yaliyotokea, nasikitika nimeshindwa kupata fulsa hata kidogo ya kufurahia mapenzi nikiwa na wewe, Najuta sana mimi kuwa chanzo cha hukumu ya mauti kwako…………, Eeh mwenyez mungu naomba unishushie rehema zako………. Naomba unipe nafasi hii ya kuishi na Tarick tukiwa peponi eeh mola wangu………… ” Brenda anabubujikwa na machozi bila kukata huku akiitizama picha ya Tarick. Anachukua karatasi kubwa na kalamu ya wino kisha anaonekana akiandika ujumbe fulani kwa umakini mkubwa,huku akiendelea kuwazua, kichwani kwake”Tarick wangu……. Napenda uniamini , Nilikuahidi kuwa sitakuacha peke yako, lakini sina nguvu ya kupambana na wenye mamlaka ili kuudhihirishia ulimwengu kuwa huna kosa”. Huku akiwa ameshikilia picha ya tariki mkononi, Anachukua vidonge vya sumu na kunywa, Baada ya hapo, Brenda analala kitandani…… na kuendelea kuandika huku akijisemea, ”Mimi natangulia mpenzi wangu”, najua utafurahi ukinikuta mpenzi wako nimetekeleza ahadi yangu”. Akiwa anatafakari maneno hayo kwa sauti ya chini huku akitoa tabasamu jepesi lililoambatana na mtiririko wa machozi Brenda anatamka,”Tarick wangu, najua uatanisamehe yote yaliyotokea ili tuanze maisha mapya tutakapo kutana tena kwenye ulimwengu wa haki…….”.

Mpenzi msomaji Baada ya Brenda kusema maneno hayo anaishiwa nguvu na kutupa peni chini.
*******************************************************************************************************************************************Wakati Mrembo Brenda akiwa anafanikisha zoezi  la kujitanguliza mbele za haki. Frank tayari alikua ameshatua Jijini Dar es salaam na mguu wake wa kwanza ulikua kwa mama, Wakati frank anaingia kwa mama ilikua ni masaa machache tu tangu, mrembo Brenda atoke mahali hapo. Frank anagonga hodi mara moja, na kabla hajaitikiwa anaingia moja kwa moja mpaka sittingroom, Nifuraha ilioje kwa mama kumuona Frank mahali pale, alikua ni kama mkombozi na mfariji pekee aliyesalia katika kipindi hiki kigumu. Mama anampokea Frank kwa furaha na majonzi, kisha anampa mkanda mzima jinsi ilivyokuwa mpaka Tarick kutiwa hatiani, Taarifa za mama zinaonesha kuwa mhusika mkubwa wa mpango huu ni Brenda, tena mama anamsimulia kwa uhakika kutokana na ushahidi ambao Brenda aliutoa Mahakamani na kumtia hatiani Tarick.

Frank anachanganyikiwa kabisa na kushindwa kujua wapi aanzie, kwani Mpaka anaondoka Tanzania Frank anakumbuka kuwa, Brenda ni msichana ambae alikua anampenda Tarick, kiasi kwamba asipomuona kulikua hakuliki wala hakulaliki, anafikiria kwa haraka haraka jinsi Brenda alivyokuwa akiwamwaga baadhi ya watu mashuhuri kwaajili ya Tarick, nini kimetokea mpaka kufanya mambo yote haya. Bila kupoteza muda anamuaga mama na kuelekea kwa Brenda.

Huku nyumbani kwa Brenda ghafla anaingia Professa Rweyemamu na kumkuta Brenda akiwa amejawa na mapovu mdomoni, Mpenzi msomaji hili linakuwa pigo la kipekee kabisa kwa profesa Rweyemamu, Hali inayompata kushuhudia mwili wa Brenda pale chini inathibitisha wazi kuwa mapenzi hayana degree wala masta, uprofesa wake wote unakuwa sifuri, analia kwa kuhamaki na kuchanganyikiwa, anatapatapa kumuamsha Brenda bila mafanikio, huku akiwa aamini anachokiona, jicho linamtoka! Uprofesa wake unashindwa kuzuia hisia nzito za mapenzi, anatiririkwa na machozi na kupigwa na bumbuwazi. Akiwa bado hajajua cha kufanya Profesa Rweyemamu analiona karatasi ambalo Brenda alikua akiliandika, Karatasi hilo lilikua likielezea nijinsi gani Profesa Rweyemamu alitumia vibaya madaraka kumtia hatiani Tarick, Karatasi hilo lilielezea jinsi Profesa Rweyemamu alivyomteka nyara mama yake na Brenda na kumlazimisha Brenda kutoa ushahidi Kama watakavyo muelekeza la sivyo wange muua mama huyo na asingeweza kuuona hata mwili wake, Karatasi hilo liliweka wazi maovu yote ya Profesa Rweyemamu katika sakata zima la kumtia Tarick hatiani.

Baada ya kulisoma karatasi hilo Profesa Rweyemamu anashukuru, kwakuwa lingeingia mikononi mwa watu wengine lingekuwa kasheshe Jipya. Wapambe wake, wanamsaidia kumnyanyua na kumuomba waondoke mahali pale, Rweyemamu analichanachana karatasi lile na kulitupia nje, kisha anaondoka na wapambe wake. Sekunde kumi na Tano Baada ya Kundi la profesa Rweyemamu kutoweka eneo hilo, anaingia Frank Naye Kama Kawaida anapigwa na butwaa, kisha anasema,”Haya ni mauaji! ”, anashindwa kupata jibu la haraka haraka, lakini kwa kuangalia mazingira anagundua kuwa kunakundi la watu limetoka mahali hapo dakika chache zilizopita. Frank anamshika shingoni kwa umakini na kugundua kuwa Brenda hakuwa amekata roho, Anatoka kwa kasi mpaka nje ili awezekufatilia kuwa ni wakina nani wametoka mahali hapo, lakini kabla hajatoka nje ya geti kabisa, anasita na kupata wazo, wakati anageuza ili arudi ndani, anaziona karatasi zilizochanwa chanwa na kukunjwa kunjwa dk chache zilizopita, zikiwa zinajikunjua na kupeperuka.

Frank Anavua kibegi alichokuwa amekivaa mgongoni na kutoa groves za kuvaa mkononi anazivaa kisha Anakusanya Karatasi hizo Haraka haraka nakuingia ndani, anafungua chumba cha kulala cha Brenda, halafu anaonekana akipekua kitu kwenye nguo za brenda.

Muda huo Prof Rweyemamu anafika ofisini kwake na kuwapa taarifa askari juu ya kifo cha Brenda anawaambia kuwa Brenda ameuwawa kwa kutumia sumu, pia anawataarifu kuwa yeye ni mtu wa kwanza kufika eneo la tukio hivyo wakiitaji msaada wowote au karatasi iliyoandikwa na marehemu kwaajili ya ushahidi anaweza kuwapatia. Ndani ya muda huo Rweyemamu tayari alikuwa amefoji karatasi nyingine iliyokuwa na maelezo yaliyokuwa yakimhusisha Tarick na kifo cha Brenda. Polisi wanapokea Taarifa hizo na kuanza safari ya kuelekea eneo la tukio.

Chumbani kwa Brenda Frank anapata Dela na kulivaa kisha anachukua kanga na kujitundika kichwani. Frank Anambeba Brenda Mgongoni na Kutoka nae nje chapchap, Sio rahisi kufikiria kuwa ni Kitu Gani frank anawaza mpaka kuamua kuvaa nguo za kike lakini inawezekana Frank akawa na maana kubwa kichwani kwake. Frank anapishana kidoogo na Maaskari ambao wanaizingira nyumba ya Brenda Dakika Chache Baada ya yeye Kutoka. Askari wanafika ndani ya nyumba hiyo na kuambulia patupu.

Frank anatokomea Mafichoni akiwa na Brenda Ambae sumu ilikua imeshamtafuna mwili mzima na muda wowote angeweza kukata roho kabisa. Akiwa kwenye maficho hayo ya siri kabisa, Frank anawasiliana na rafiki yake Dokta Roby na kumuacha akiwa ameanza matibabu ya Brenda maramoja, ili kuona kama anaweza kuunusuru uhai wa mrembo huyo. Baada ya hapo Frank anarudi nyumbani na kumliwaza mama kuwa asiwe na hofu siku mbili zilizo salia atajaribu kufanya kila linalowezekana ili akate rufaa. Usiku kucha wa siku hiyo Frank alikaa macho akijaribu kuunganisha vipande vya makaratasi, Frank anashindwa kupata ujumbe uliokuwamo ndani ya karatasi zile lakini anapata mwangaza na kuona jina la mh profesa rweyemamu japokuwa anashindwa kusoma kuwa linahusika na nini, Frank anamfikiria Brenda kuwa angekuwa na fahamu angesema chochote. anaamua kuvikunja vizuri vile vikaratasi na kuvihifadhi.

Siku inyofata Alfajiri, Frank anaelekea mahakamani ili akakate rufaa, Frank anafika mahakamani na kuambiwa kuwa imekuwa vizuri amewahi kwani saa sita ndio mwisho wa rufaa na hati za hukumu sinasafirishwa saa 8 kuelekea Dodoma. Kwakuwa ilikua bado mapema alfajiri, Frank anafanya mpango nakutafuta wakiri ili amsaidie kwenye zoezi zima la kukata rufaa. Taarifa za kwamba kunamtu aliejitambulisha kama ndugu yake na Tarick na anafanya mchakato wa kukata rufaa zinamfikia Profesa Rweyemamu, Haraka haraka Profesa Rweyemamu anawasiliana na Baadhi ya viongozi wa mahakama, kisha wanafunga rufaa kabla ya muda, halafu hati za hukumu zinasafirishwa kuelekea Dodoma, kwenye gereza la Isanga ambako Frank pamoja na watu wengine 9 wenye kesi za ugaidi na mauaji katika matukio matatu tofauti watanyongwa huko.

Baada ya Frank na mwanasheria Wake Kuhangaika kwa muda, Wanakamilisha Maandalizi ya stakabadhi zote na kuzipeleka mahakamani. Hapo Frank anapewa taarifa kuwa Rufaa ilikua tayari imesha fungwa na Hati za hukumu zimesafirishwa kuelekea Dodoma, hivyo haito wezekana tena kukata rufaa. Frank anaonekana akitafakari jambo kwa makini, lakini kitu cha kushangaza nikwamba, hakuonesha hofu wala wasiwasi, anakua kama mtu alietarajia kinachoendelea. Wakili wake anamwambia,”Pole mista Frank, Nasikitika kuwa hili limesha shindikana…..” Frank anamtizama wakili wake, kisha anatoa tabasamu jepeeesi na kumjibu,”Usijali, I’m going to turn the next side of this coin” baada ya maneno hayo anamlipa wakili wake na kuachana nae.

Mpendwa msomaji unaefatilia kisa hiki cha kusisimua, Kumbuka nilikwambia kuwa Frank kipindi cha ukuaji wake alikua ni mtu mwenye uwezo mkubwa wa kufikiria, na ujasiri mkubwa, mtu ambae hana hofu anapofanya jambo lolote, Ujasili huu ndio uliopelekea mpaka jamaazake aliokuwa nao kumpa jina la Samba. Baada ya kuona Plan ya kwanza imeshindwa, anamuahidi wakili wake kuwa kinachofata sasa ni kugeuza mchezo kwenye upande wa pili wasarafu nini kitafatia!?Usikose kuungana nami katika episode ya 3 ya Tamthilia hii ya kusisimua.

0 comments:

Post a Comment